Jumapili 4 Oktoba 2026 - 08:30
Kumbukumbu Zenye Kuvutia za Ayatullah Tabasi Kumhusu Kiongozi Shahidi

Hawza/ Ayatullah Tabasi, akisimulia kumbukumbu zake kuhusu kukutana na Kiongozi Shahidi, amesema: Katika moja ya mikutano hiyo, ilitokea fursa ya kuwasilisha ombi la kusitisha uuzaji na usambazaji wa machapisho ya Ibn Taymiyyah katika maonesho ya vitabu nchini Iran, na kutolewa agizo la kufuatilia suala hilo. Miaka kadhaa baadaye, niliona athari za hatua hiyo katika mojawapo ya maduka ya vitabu mjini Beirut.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Najmuddin Tabasi, mwalimu wa masomo ya juu ya nje (Darsul-Kharij) katika Hawza na mjumbe wa Jumuiya ya Walimu wa Hawza ya Qum, katika mahojiano yake na mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza mjini Qum, akizungumzia mikutano kadhaa aliyokutana na Kiongozi Shahidi, Ayatullah al-Udhma Imam Sayyid Ali Khamenei (Mwenyezi Mungu aitakase roho yake tukufu), alisema: “Katika mikutano hiyo, nilimwona akiwa amejawa na unyenyekevu, adabu, maadili mema, maarifa na kujali watu. Sitasahau kamwe heshima aliyokuwa akiwaonesha watu wote, hususan wanafunzi wa Hawza.”

Simulizi Kuhusu Unyenyekevu wa Kiongozi Shahidi Katika Mkutano wa Kielimu

Akizungumzia mojawapo ya mikutano hiyo, iliyofanyika sambamba na kumbukumbu ya kuuawa kishahidi Imam Hasan al-Askari (as), aliongeza: “Kulikuwa na kikao cha faragha katika ofisi yake, kilichohudhuriwa na watu wapatao 200 hadi 300, nami pia nilihutubia katika kikao hicho kwa takribani dakika 40. Baada ya kumalizika hotuba yangu, Kiongozi Shahidi alizungumzia baadhi ya hoja nilizokuwa nimeziwasilisha, kisha tukazungumza pamoja kwa takribani dakika 40 hadi 50. Baadaye, tulijadili kuhusu Ibn Abbas na masuala mengine, kisha akakitaja kitabu ‘Al-Nafyu wa al-Taghrib’ na kusema kwamba kitabu hicho ni kizuri, kina vipengele vya kifiqhi na kihistoria, na kwamba alikuwa amekisoma kuanzia mwanzo hadi mwisho.”

Ayatullah Tabasi alisisitiza kwamba Kiongozi Shahidi alieleza kuwa, licha ya majukumu na shughuli nyingi alizokuwa nazo, alikuwa amekisoma kitabu hicho kuanzia mwanzo hadi mwisho. Hata miaka kadhaa kabla ya hapo, alikuwa amekisoma kitabu hicho chote.

Mwalimu wa Hawza ya Qum aliendelea kusema: “Katika mkutano huo, nilikuwa pia na kitabu kingine kilichohusu mihadhara na maelezo ya masomo ya juu ya fiqhi (Taqrirat al-Kharij), ambacho kilikuwa bado hakijachapishwa. Nilikuwa na nakala yake iliyochapwa kwa mashine ya kuandika. Nilimwonyesha kitabu hicho, naye Kiongozi Mkuu akakichukua kutoka kwangu kwa ajili ya kukisoma na kutoa maoni yake.”

Kumbukumbu ya Kitabu ‘Jela Katika Uislamu’ na Jinsi Kiongozi Shahidi Alivyokisoma Mara Kadhaa

Akisimulia kumbukumbu yake ya pili, Ayatullah Tabasi alisema: “Mkutano mwingine ulifanyika mwaka 1372 Hijria Shamsia \[1993–1994 Miladia\], takribani miaka 33 iliyopita. Wakati huo, nilimtumia Kiongozi Shahidi kitabu changu kilichoitwa ‘Jela Katika Uislamu’. Baada ya kukituma, niliwasiliana na Ofisi ya Kiongozi na kueleza kwamba nilipenda kufahamu maoni yake kuhusu kitabu hicho. Baadaye, nilijulishwa kutoka ofisini kwamba Kiongozi Mkuu alitaka kuniona, hivyo nikaenda kukutana naye.”

Mwalimu wa Hawza ya Qum aliongeza: “Siku hiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kukutana naye. Kikao hicho kilihudhuriwa na watu wapatao 20 hadi 30, na wakati fulani kikao kiligeuka kuwa cha faragha zaidi. Katika hatua hiyo, alinizungumzia kuhusu kitabu changu.”

Akizungumzia yaliyomo katika mazungumzo hayo, alifafanua: “Kiongozi Shahidi alisema kwamba alikuwa amekisoma kitabu hicho mara nne au tano, kuanzia mwanzo hadi mwisho.”

Ayatullah Tabasi, akizungumzia ukubwa wa kitabu hicho, alisema: “Kitabu hicho kilikuwa na takribani kurasa 700 hadi 800. Alisisitiza kwamba alikuwa amekisoma kuanzia mwanzo hadi mwisho, na akakielezea kuwa ni kitabu cha marejeo chenye umuhimu mkubwa na kinachostahili kuzingatiwa.”

Mwalimu wa masomo ya juu ya nje katika Hawza alibainisha kwamba baadaye, marehemu Ayatullah Yazdi pia alizungumzia kitabu hicho katika khutba ya kwanza ya Swala ya Ijumaa. Baada ya hapo, alimwambia Ayatullah Tabasi kwamba kabla ya kutoa khutba hiyo, alikuwa ameketi na kuzungumza na Kiongozi Shahidi kuhusu kitabu hicho.

Aliongeza: “Ayatullah Yazdi alisema kwamba walikuwa wamezungumzia kitabu hicho katika kikao hicho, na baadaye maudhui yake yakawasilishwa katika khutba ya kwanza ya Swala ya Ijumaa.”

Kuzuia Usambazaji na Upatikanaji wa Machapisho ya Ibn Taymiyyah

Akizungumzia mwendelezo wa mkutano huo, Ayatullah Tabasi alisema: “Umakini na heshima ambayo Kiongozi Shahidi aliionesha kwenye kitabu hiki vilikuwa na thamani kubwa sana kwangu. Nilihisi kwamba alikuwa amekipa kitabu hicho uzito na umakini ambao nilikuwa nikitarajia.”

Aliongeza: “Baadaye, nilimweleza kwamba kuhusu Ibn Taymiyyah na machapisho yake, hata baadhi ya wanazuoni wa Ahlus-Sunna wameeleza maoni ya kumpinga na kumkosoa. Baadhi yao humtaja Ibn Taymiyyah mwenyewe kuwa ni zindiki na mtu aliye nje ya dini. Hata hivyo, licha ya hayo, bado kulikuwa na mazingira yaliyowezesha watu kupata na kununua machapisho yanayomhusu katika masoko. Kwa hiyo, niliomba kwamba atoe agizo la kusitisha usambazaji wa vitabu vya Ibn Taymiyyah.”

Alibainisha kwamba Kiongozi Shahidi aliuliza ikiwa vitabu hivyo vilikuwa vinapatikana sokoni au la. Ayatullah Tabasi akamjibu kwamba Wizara ya Utamaduni na Mwongozo wa Kiislamu ndiyo iliyokuwa imevileta vitabu hivyo kwa ajili ya maonyesho ya vitabu. Alisema kwamba Kiongozi Shahidi alikasirishwa sana na jambo hilo, kisha akamwagiza Bwana Muhammadi aandike suala hilo na kulifuatilia.

Niliona Matokeo ya Msaada wa Kielimu Baadaye Mjini Beirut

Akiendelea na simulizi yake, Ayatullah Tabasi alisema: “Miaka kadhaa baadaye, nilipokwenda Beirut, nilikuwa katika mojawapo ya maduka ya vitabu yaliyoko katika eneo la Dhahiyah. Hapo nilisikia muuzaji mmoja wa vitabu akizungumza na mwenzake kuhusu hali ya vitabu vya Ibn Taymiyyah katika maonyesho ya vitabu nchini Iran. “Muuzaji huyo alisema kwamba mwaka huo, kila vitabu vya Ibn Taymiyyah vilipowekwa katika banda lolote kwenye maonyesho ya vitabu nchini Iran, hatua zilichukuliwa dhidi yake na usambazaji wake ulizuiwa. “Niliposikia maneno hayo, nilijiambia moyoni: Alhamdulillah! Nimepokea tuzo yangu. Yaani, msaada niliouomba kutoka kwa Kiongozi Shahidi ulikuwa umetimia.”

Kumbukumbu ya Mkutano wa Mwisho

Mwisho wa simulizi yake, Ayatullah Tabasi alizungumzia mkutano wake wa mwisho na Kiongozi Shahidi, akisema: “Katika kikao hicho, nilipotaka kumbusu mkono wake, hakuniruhusu. Nilimweleza kwamba Kiongozi Mkuu, Sayyid, ni miongoni mwa kizazi cha Mtume wa Mwenyezi Mungu (saww), ni mwanazuoni na faqihi, na ana sifa zote hizo. Hata hivyo, pamoja na yote hayo, hakuniruhusu kumbusu mkono wake. “Bila shaka, baada ya kujitahidi sana, nilifanikiwa kumbusu mkono wake wa juu, karibu na kiwiko, na ninajivunia kwamba nilifanya hivyo.”

Mwalimu wa Hawza ya Qum alihitimisha kwa kusisitiza kwamba; mambo yaliyomvutia zaidi katika mikutano hiyo yalikuwa ni unyenyekevu wa Kiongozi Shahidi, adabu yake, maadili yake mema, maarifa yake, kujali kwake watu na heshima aliyokuwa akiwaonesha watu wote, hususan wanafunzi wa Hawza.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha